Genesis 50

1Basi Yusufu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu. 2Ndipo Yusufu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa ili asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze, 3wakatumia siku arobaini, kwa maana ndio muda uliotakiwa wa kutia dawa ili asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.

4Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yusufu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni, 5‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ”

6Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”

7Hivyo Yusufu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake na watu mashuhuri wote wa Misri. 8Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani kwa Yusufu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni. 9Magari makubwa na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.

10Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu; Yusufu akapumzika huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake. 11Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.
Abel-Mizraimu maana yake Maombolezo ya Wamisri.

12Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza: 13Wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Ibrahimu alilinunua kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia. 14Baada ya Yusufu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake.

Yusufu Awaondolea Ndugu Zake Mashaka

15Ndugu zake Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yusufu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” 16Kwa hiyo wakampelekea Yusufu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: 17‘Hili ndilo mtakalomwambia Yusufu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yusufu akalia.

18Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”

19Lakini Yusufu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? 20Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. 21Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.

Kifo Cha Yusufu

22Yusufu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110, 23naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yusufu walipozaliwa.

24Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Ibrahimu, Isaka na Yakobo.” 25Naye Yusufu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”

26Kwa hiyo Yusufu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.
Copyright information for SwhKC